Katika maisha, kila siku tunatengeneza na kuvunja urafiki na watu wanaotuzunguka. Wengine wanatuachia mafunzo mazuri, wengine tunawaachia mafunzo mazuri pia, pia wapo wanaojivika ngozi ya kondoo kumbe ni mbwa mwitu wakali wanaotutafuna na kuturudisha nyuma kila siku.
Pamoja na hayo yote, bado tunahitaji watu wachache watakaoifanya safari ya kutafuta mafanikio na kuleta mabadiliko katika maisha yetu iwe yenye Thamani, kuleta Tabasamu na Furaha zaidi. Hawa ni watu watakuwa na wewe katika hali zote hata bila kujali mazingira waliyopo, watajitahidi kuchangia kwa namna moja au nyingine katika kuhakikisha unakuwa bora zaidi kila siku.
Hivyo basi, leo nitakufahamisha aina 6 za watu wanaopaswa kuwepo katika mfumo wako wa maisha ya kila siku. Baada ya kumaliza kusoma makala hii, naomba usisahau kumtafuta rafiki yako nwenye sifa hizi na kumweleza umuhimu wake katika maisha yako.
1. Watu/marafiki wanaokusukuma kusonga mbele zaidi.
Hawa ni watu muhimi sana katika maisha yetu. Ni aina ya watu watakaosimama na wewe katika mazingira yote na kuhakikisha unasonga mbele. Sifa kubwa ya watu wa aina hii ni kwamba, watakuamini zaidi hata pale utakaposhindwa kujiamini wewe mwenyewe. Watakupa hamasa ya kutimiza malengo yako hata pale utakapohisi kukata tamaa au kushindwa kuendelea mbele.
2. Mtunza siri zako (Mwaminifu)
Huyu ni mtu muhimiu sana kwako. Mtu atakaye kusikiliza bila vikwazo vyovyote na sio mwepesi wa kuhukumu bila sababu. Unapopata misukosuko mbalimbali, huyu ndiye mtu wa kwanza kuongea nae na kujisikia amani pale unapomuelezea changamoto zako. Huyu ni rafiki wa kuwa nae daima. Atakusikiliza na kutengeneza mazingira huru ya kuzungumza. Mpe THAMANI kubwa sana mtu wa aina hii. Unapaswa kuwa rafiki mzuri sana na mwaminifu pia pale utakapompata rafiki wa aina hii.
3. Mshauri wako.
Kuna wakati utajikuta hauna elimu/ujuzi wa kutosha katika baadhi ya mambo. Lakini ni rahisi zaidi kupiga hatua pale unapokuwa na mtu wa kukushauri na kukuongoza kupita njia iliyo sahihi. Ni muhimu sana kuwa na mtu wa aina hii kutokana na experience yake juu ya changamoto unayoipitia. Utapunguza asilimia kubwa ya kufanya makosa madogo madogo kwa sababu atakuwa ni kiongozi wako kutoka na experience yake. Mshauri wako anaweza kuwa ni Mwalimu wako, Mzazi/mlezi wako au hata rafiki yako mwenye experience kukuzidi wewe.
4. Rafiki wa muda wote.
Katika maisha yetu, wapo marafiki ambao wao, haijalishi wapo katika mazingira gani ila inapotokea unawahitaji , basi wanakuja kukaa na wewe bila kuuliza uliza maswali. Mara nyingi marafiki wa aina hii huwa tunawachukulia kama “Machizi” kutokana na vituko vyao na namna wanavyoleta Furaha na Tabasamu katika maisha yetu. Unahitaji watu wa aina hii kwa sababu wataendelea kuhakikisha unapata Furaha na kutabasamu zaidi katika maisha yako.
5. Rafiki wa Dhati (Best Friend)
Sio kila mtu anafaa kuwa Best Friend wako. Rafiki wa Dhati [Best Friend] anabeba sifa zote/kiasi kikubwa cha sifa za watu unaopaswa kuwa nao kama nilivyoelezea hapo juu [Aina ya 1-4]. Mtu wa aina hii sio lazima sana awe jinsia moja na wewe. Mtu wa aina hii yupo radhi umchukie na kumuona mbaya lakini atasimama katika kukuambia ukweli pale unapohitaji kuambiwa ukweli, atakukosoa na kuhakikisha unarudi katika mstari sahihi pale unapokosea.
Katika mazingira yote, watu wa aina hii wanajua namna ya kukufanya uwe na Furaha, wanakutunzia siri zako na kubwa zaidi wanafahamu njia sahihi zaidi za kukupa hamasa ya kusonga mbele. Kwa kifupi mtu wa aina hii tunasema anakufahamu “Nje Ndani” yaani “Hakuna asichokijua kuhusu wewe.”
“Kaa Karibu na watu sahihi katika maisha yako ili uweze kuvutia fikra chanya zitakazo kusaidia kusonga mbele zaidi.”
Natumaini makala hii itakusaidia kuchagua aina ya watu unaopaswa kuwa nao kila siku katika maisha yako. Mwenyezi Mungu akusaidie na kukuongoza katika kuwapata watu wa wa aina hizo katika maisha yako.