Kuna uwezekano mkubwa umewahi kusikia kuhusu malengo, Umewahi kusikia juu ya nguvu iliyopo katika malengo, umewahi kusikia pia aina mbalimbali za malengo. Lakini bado unapata ugumu na unashindwa kufahamu ni wapi uanzie ili kujiwekea malengo na kuyatimiza.
Kabla haujaanza kuweka malengo, unapaswa kwanza kufahamu aina za malengo kutokana na mahitaji yako na muda uliopo. Kuna aina kuu mbili za malengo unazopaswa kuzifahamu;
- Malengo kwa kuzingatia kigezo cha muda.
- Malengo kwa kuzingatia vipengele 7 muhimu katika maisha.
Kama bado una wasiwasi juu ya aina za malengo na namna gani unaweza kuweka malengo yanayokidhi mahitaji yako, basi upo sehemu sahihi kabisa. Makala hii itaondoa kabisa wasiwasi wako na mwisho utafahamu ni aina gani ya malengo yanaweza kukidhi mahitaji yako. Tuanze kwa kuangalia Mtazamo wa watu wengi kuhusu kujiwekea malengo.
UNA MTAZAMO GANI KUHUSU KUWEKA MALENGO?
Hebu tuangalie kwanza maana au uelewa halisi juu ya Malengo. Asilimia kubwa ya watu hudhani Kwamba, Malengo ni lazima kiwe ni kitu kikubwa sana, ni lazima ufikie mafanikio makubwa ndio uweke malengo au upate pesa nyingi ndio uanze kuweka malengo.
Sio sahihi kabisa!
Malengo sio lazima ufikie mafanikio makubwa katika maisha yako, sio lazima uwe na pesa nyingi ndio uanze kuweka malengo. Wakati wowote ule unapohitaji kutimiza jambo fulani, basi utakuwa sahihi kabisa ukiweka malengo ya namna ya kukitimiza au kukifikia.
Kumusi ya Merriam-Webster inasema kwamba “A goal is something that you are trying to do or achieve.”
Kwa tafsiri isiyo rasmi maana yake ni kwamba, “Lengo/Malengo ni kitu chochote unachotamani/kuhitaji kufanya au kukifanikisha.” Kwa maana hiyo, sio lazima kiwe ni kitu kikibwa sana bali “Ni kitu chochote”, kiwe ni kidogo au kikubwa.
AINA NNE ZA MALENGO KWA KIGEZO CHA MUDA.
Pale unapoweka malengo, Muda utakaotumia ni moja ya kitu muhimu sana cha kuzingatia. Kutokana na kigezo hiki, kuna aina nne za malengo;
- Malengo madogo madogo (Ya kila siku).
- Malengo ya muda mfupi.
- Malengo ya muda mrefu.
- Malengo ya Maisha yako.
4. MALENGO YA MAISHA YAKO
Malengo ya maisha yako ni malengo yanayoweza kuchukua miaka 10 na zaidi ili kuyatimiza. Malengo haya ndio kusudi halisi la kila unachokifanya katika maisha yako. Njia nyepesi na rahisi ya kutambua malengo yako ya maisha, ni kutazama maono/maisha yako ya baadae. Unataka kuwa nani au mtu wa aina gani miaka ijayo?
Katika Maono yako, tafuta majibu sahihi ya maswali haya;
- Umefanikiwa kukamilisha nini?
- Je, ulikuwa na Furaha?
- Je, Utakuwa katika Familia au bado ukiwa peke yako?
- Je, katika maono yako, utafanikiwa kwa kiasi gani?
- Utabadilika au utakuwa vile vile kama ulivyo sasa?
- Utakapoondoka hapa duniani, watu watasema nini juu yako?
Unapotazama na kufikiri juu ya “Wewe wa Baadae” (Maono yako) na kuweka mwanga huu, tayari unatengeneza mahala pa kuanzia katika kuweka malengo yako. Haya ni malengo yanayoelezea juu ya hatima ya maisha yako. Ukishayafahamu maono yako, basi weka malengo ya kubadilika na kuwa mtu yule uliyemtazama katika maono yako.
3. MALENGO YA MUDA MREFU.
Malengo haya ni sawa na kitendea kazi chako. Maana yake ni kwamba, malengo haya utayatumia ili uweze kufika katika malengo yako ya maisha. Mara nyingi malengo ya aina hii yanahitaji muda maalumu wa kuyatimiza, na mara nyingi huwa si chini ya miaka 3. Mfano: Unaweza kusema,
- “Nataka kuweka akiba ya Tsh Millioni 50 kabla sijastaafu kazi kufikia mwaka 2025.”
2. MALENGO YA MUDA MFUPI.
Malengo ya aina hii huchukua, mwezi 1, miezi 3, 6 au mwaka mzima. Malengo haya husaidia katika kuyafikia malengo ya muda mrefu na mara nyingi hutokana na malengo madogo madogo. Mfano: Tuendelee katika mfano wa “kuweka akiba ya Tsh Millioni 50 mpaka mwaka 2025.”
Kama lengo lako ni kuweka akiba, basi malengo yako ya muda mfupi yanaweza kuwa;
- “Kutumia Bank yenye makato madogo zaidi kuweka akiba yako.”
- “Kulipa madeni na mikopo ya Bank unayodaiwa.”
1. MALENGO MADOGO MADOGO
Haya sasa, ni malengo ya kila siku. Inahusisha ratiba na mwenendo wako wa kila siku. Malengo haya ndio yatakyokuwezesha kufikia malengo ya muda mfupi, mrefu na mwisho malengo yako ya maisha kwa ujumla. Mfano: Kutoka katika moja ya malengo ya muda mfupi “Kulipa madeni na mikopo yako ya Bank”. Malengo yako madogo madogo yanaweza kuwa;
- “Kuhudhuria semina juu ya Kuweka akiba na kuweka bajeti.“
- “Kupunguza idadi ya matumizi katika maisha yako.”
- “Kupata kazi ya Ziada itakayokusaidia kuongeza kipato chako.”
- “Kulipa madeni yako angalau kila mwezi.“
MALENGO KWA KUZINGATIA MAENEO 7 MUHIMU KATIKA MAISHA
Maisha yetu kama binadamu yamegawanyika katika maeneo 7 muhimu. Kila eneo linahitaji kuwa bora zaidi ili kuongeza THAMANI zaidi katika maisha yako. Njia pekee ya kufanya hivyo, ni kuweka malengo. Maeneo hayo 7 ni haya;
1. KAZI
Una malengo gani katika kazi yako? Unataka utambulike kama nani katika jamii yako? Ni vyema sana kuweka malengo mbalimbali kwa kuzingatia kazi au majukumu yako ya kila siku. Mfano wa mambo ya kuzingatia hapa ni pamoja na;
- Kujifunza ujuzi mpya unaoendana na kazi yako.
- Kupandishwa cheo.
- Kujiajiri kwa kuanzisha biashara yako mwenyewe.
- Kuongeza mapato zaidi kwako mwenyewe au katika kampuni unayofanyia kazi n.k.
2. UCHUMI
Hapa ni sehemu muhimu sana katika kujiwekea malengo.
“Asilimia kubwa ya watu wanapenda kupata pesa lakini ni wachache sana wanaweka malengo na mipango ya kuipata.”
Anselmo John
Ili kufikia malengo yako kiuchumi unapaswa kuzingatia sana suala la bajeti, kupangilia matumizi yako na kujenga tabia ya kujiwekea akiba. Baadhi ya mambo ya kuzingatia ili kufikia malengo yako ya kiuchumi ni pamoja na;
- Kulipa/Kupunguza madeni.
- Kuwa na mfuko wa akiba.
- Kujiwekea pesa ya dharura.
- Kununua Assets mbalimbali nk.
3. KIROHO
Una utaratibu gani juu ya maendeleo au ukuaji wako kiroho. Ni muhimu sana kuzingatia ukaribu wako na Muumba wako (Mwenyezi Mungu). Haya ni malengo unayoweza kujiwekea pasipo kuangalia dini au dhehebu lako. Kila mmoja anamuhitaji Mungu katika maisha yake. Baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia hapa, ni pamoja na;
- Kwenda eneo lako la kufanyia ibada kulingana na utaratibu wa imani yako.
- Kujitolea katika shughuli mbalimbali za kidini.
- Kujiunga katika vikundi mbalimbali vya kiroho.
- Kusoma neno la Mungu kila siku.
- Kuwa mtu wa sala mara kwa mara.
- Kujitolea katika kusaidia wale wenye uhitaji bila kutegemea malipo nk.
4. ELIMU/MAARIFA
Unahitaji maarifa zaidi katika maisha yako. Iwe ni kwa kupitia mfumo wa kwenda darasani au kutafuta maarifa binafsi. Elimu/Maarifa yanahitajika sana katika maisha yako. Jambo la kuzingatia ni kwamba, “Maarifa/Elimu hiyo iendane kwa kiasi kikubwa na kazi yako au unayotarajia kuifanya hapo baadae.”
Malengo ya kielimu/Maarifa yanatofautiana kulingana na mahitaji ya mtu mwenyewe. Kikubwa hapa ni kuhakikisha unapata Elimu/Maarifa sahihi kwa wakati sahihi.
5. FAMILIA & MAHUSIANO
Usishangae! Ndio, unahitaji kuweka malengo katika mahusiano na Familia yako pia. Aina yoyote ile ya mahusiano, inahitaji malengo ili kuongeza zaidi ustawi wake. Ninasema hivi kwa sababu, moja kati ya sababu ya mahusiano mengi na baadhi ya Familia kuvunjika/kuharibika ni “Kukosa Malengo.” Malengo husaidia kuweka uhai wa mahusiano yoyote na kujenga ukaribu kwa wanafamilia. Usichukulie poa suala hili.
Baadhi ya mambo ya kuzingatia hapa ni pamoja na;
- Kutenga Muda kwa ajili ya Familia yako.
- Kuboresha mawasilino baina yako na Rafiki, mpenzi, mke au watu wako muhimu.
- Kupata watoto.
- Kufunga ndoa nk.
6. AFYA
Afya yako ni muhimu sana pia. Waswahili wanasema, “Afya ni Mtaji”. Ni ngumu sana kufanya jambo lolote katika ufanisi ikiwa afya yako inatetereka. Weka tabia na utaratibu wa kujali afya yako pasipo kusubiri ushauri wa daktari. Haya ni baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia;
- Kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi.
- Kufanya check-up ya afya yako mara kwa mara.
- Kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari nyingi.
- Kula mlo bora kwa wakati sahihi nk.
Mpaka hapo, ni imani yangu umepata mwanga wa namna ya kuweka malengo kulingana na mahitaji yako kwa kuzingatia maeneo mbalimbali muhimu katika maisha yako. Dhumuni kubwa hapa, si kuweka malengo katika eneo moja, bali kujiwekea malengo kwa kuzingatia kila eneo muhimu katika maisha yako.