Mitandao ya Kijamii ni miongoni mwa njia nzuri sana zinazoweza kukusaidia kuongeza mauzo katika Biashara yako. Lakini, mpaka leo, bado kuna wafanyabiashara wachache wanaamini hakuna umuhimu wowote wa kuwekeza muda na pesa katika mitandao ya kijamii ili kukuza zaidi Biashara na Huduma zao.
Katika uhalisia, mitandao ya kijamii imeleta mageuzi makubwa katika Biashara duniani kote, ni eneo linaloweza kukusadia kupiga hatua Zaidi katika Biashara yako, kama tu utajifunza namna ya kuitumia kwa usahihi.
Hata hivyo, pamoja na Kwamba mitandao yote ya kijamii ina faida na umuhimu wake, katika makala ya leo tutaangalia Zaidi mtandao wa Instagram, na kwa namna gani unaweza kuutumia ili kuongeza mauzo zaidi, uwe unauza nguo, vipogozi, saa, au bidhaa nyingine yoyote.
Hizi ni mbinu 3 muhimu zitakazokusaidia kuongeza Mauzo katika Biashara yako kupitia mtandao wa Instagram.
Hakikisha unatengeneza Maudhui sahihi
Kutengeneza Mahusiano ya karibu na followers wako, ni MUHIMU sana katika kuongeza mauzo ya bidhaa zako. Moja ya njia sahihi zaidi ya kujenga mahusiano haya, ni kupitia maudhui kuhusu Bidhaa zako.
Kama unauza bidhaa inayohitaji maelezo ya ziada kwa ajili ya kumshawishi wateja wako, basi usione aibu kuwapatia maudhui yanayoeleza na kutoa taarifa sahihi kuhusu bidhaa yako.
Na katika uhalisia, kila Bidhaa ina aina ya Taarifa au Elimu inayohitaji kumfikia Mteja wako.
- Unauza Viatu: Fundisha aina mbalimbali za kufunga Kamba za viatu
- Unauza saa: Fundisha namna ya kuhifadhi saa ili idumu kwa muda mrefu
- Unauza Perfume: Fundisha aina 5 za Perfume nzuri kwa kila mwanaume
Tengeneza maudhui ya kipekee, yatakayokutofautisha na watu wengine wanaofanya Biashara au kuuza Bidhaa kama zako. Maudhui haya, yanaweza kuwa;
- Picha kuhusu bidhaa zako
- Video ukielezea kuhusu Bidhaa zako
Tumia Shududa za wateja kujenga Uaminifu Zaidi
Siku zote ni muhimu sana, kuonyesha shuhuda za watu wengine waliowahi kutumia au kununua bidhaa zako. Ukweli ni kwamba, wateja hawapendi kujiona wao ndio wa kwanza kununua bidhaa yako.
Kwa hiyo, Kila wakati utakapoonyesha watu waliowahi kununua au kutumia bidhaa yako, kupitia feedback zao nzuri au shuhuda, itakusaidia sana kuongeza uaminifu na kuondoa hofu kwa watu ambao bado hawajafanya uamuzi wa kununua bidhaa yako.
Fanya Matangazo kwa usahihi
Kama kuna eneo lenye faida zaidi kuhusu Instagram kwako wewe mfanyabiashara, basi ni kukupa uwezo wa kufanya Matangazo na kuwafikia watu wengi zaidi wasiofahamu kuhusu bidhaa au Biashara yako.
Unaweza kutengeneza Matangazo yako wewe mwenyewe, au kutumia mtaalamu atakaekusaidia ili uweze kupata matokeo mazuri Zaidi. Haijalishi ni wewe au mtu mwingine atakaesimamia Matangazo yako, jambo muhimu Zaidi ni kutambua Mlengwa wa Tangazo lako – Hii ni hatua muhimu mno.
Lakini, Hilo lisikupe wasiwasi, kwa sababu, Instagram inakupa uwezo kuchagua ni nani aone tangazo lako kulingana na tabia mbalimbali za watumiaji wa mtandao huo. Muhimu zaidi, ni wewe kama mfanyabiashara, kufahamu ni aina gani ya mteja anaweza kununua bidhaa yako.
Na katika Tangazo lako, mwambie mteja, atapata nini endapo atafanya uamuzi wa kununua, faida atakayoipata, gharama za bidhaa, pamoja na nini anapaswa kufanya ili kuipata bidhaa hiyo.
Kwa kutumia mbinu hizi 3, utawatengenezea wateja wako mazingira ya kuona wanapata faida na Thamani inayoendana na pesa wanayoitoa, na kuwashawishi waendelee kununua zaidi kutoka kwako.