Ni kweli una wazo zuri sana la biashara. Ni wazo bora mno, linakuvutia sana na kukupa hamu ya kuchukua hatua na kufungua biashara hiyo hata kesho. Yaani unatamani upate kila unachokihitaji ili uanze mara moja kufanya biashara hiyo.
Hebu subiri kidogo! Kabla hujafikiria hata kuanza kununua kifaa chochote, kusajili na kuajiri watu wa kukusaidia. Kuna maswali matatu muhimu sana unapaswa kujiuliza.
Majibu ya maswali haya yatakusaidia kutengeneza njia yako ya mafanikio na kukusaiida kuepuka stress, kupoteza pesa na muda kwa kukupa mwanga wa kutambua kama biashara unayotaka kufanya inaweza kukupa faida au lah.
Upo tayari sasa kupata maarifa haya? Haya ndio maswali 3 muhimu unayopaswa kujiuliza kabla ya kuanzisha biashara yako.
1. Kwanini unatamani kuanzisha biashara hiyo?
Unaweza kudhani ni swali rahisi au lisilo na maana kubwa. Lakini, hili ndio swali litakalokufanya ulitafute “kusudi” la kwanini na kuna faida gani ya wewe kufanya biashara hiyo.
Zaidi kabisa, ni swali litakalokupa ufunguo wa kuona usahihi wa maamuzi yako na hamasa ya kupambana kwa hali na mali ili uweze kufikia kusudi lako.
Majibu yanaweza kuwa:
- Unataka kujiajiri mwenyewe
- Unataka kuishi ndoto zako kwa kufanya kile unachokipenda
- Unataka upate pesa za kusaidia familia yako na wale uwapendao
Yote yanaweza kuwa ni majibu sahihi, kwa sababu “Kusudi” lako lazima liwe sambamba na kile unachotamani kukipata au matokeo unayotamani kuyapata kutokana na uwepo wa biashara hiyo. Kwanini hii ni muhimu?
Kwa sababu, hata pale utakapohisi kukata tamaa, utakapokutana na changamoto, majaribu na vikwazo, lile “kusudi” lako ndio litakuwa tumaini kubwa na chanzo cha hamasa itakayokusukuma kusonga mbele kwa ujasiri mkubwa.
Ndio maana, usipokuwa na kusudi sahihi kama vile “Nataka kuanzisha biashara ili kushindana na mtoto wa Shangazi”, ni ngumu sana kutoboa! Kwa sababu, pindi utakamuona mtoto wa shangazi anaendelea kukutimulia vumbi, utaanza kujenga chuki, utapoteza focus yako, na utakata tamaa haraka mno!
Jitahidi sana kutafuta “Kusudi” la dhati linalokusukuma kuanzisha biashara hiyo. Kusudi sahihi ndio litakusaidia kupenya hata pale unapodhani huwezi kuingia.
2. Unataka kutatua tatizo gani katika jamii?
Hili ni swali ambalo labda hujawahi kabisa kujiuliza au pengine huoni uzito wake kwa sababu unaona akaunti za wajasiriamali wenzako katika mitandao ya kijamii, zikiendelea kukua tu kila siku. Basi, na wewe ukatamani kuwa kama wao.
Ngoja nikusaidie tu, tena kwa sababu nzuri kabisa; endapo biashara yako haitaenda kutatua tatizo kwa mtu yeyote, basi haifai kufunguliwa. Usipoteze muda!
Kuwa na shauku kubwa juu ya wazo lako la biashara, ni vizuri na muhimu mno. Kwa sababu, usipokuwa na shauku ya kile unachokitaka wewe mwenyewe, nani atakuwa na shauku nacho?
Lakini muhimu zaidi, ikiwa hakuna mtu mwingine mwenye shauku ya kutosha kuhusu biashara yako na hayupo wa kununua bidhaa au huduma yako – basi hiyo sio biashara inayofaa au kuhitajika katika jamii yako.
Unahitaji kujiuliza maswali yafuatayo:
- Je, biashara hii inatatua tatizo gani?
- Je, biashara hii inatatua matatizo kwa ajili ya nani? (Na kuna watu wangapi wanahitaji uwepo wa biashara hii?)
- Je, watu hao wako tayari kulipa ili kupata suluhu ya matatizo yao?
- Je, wako tayari kulipa kiasi gani ili kutatua matatizo yao? (Na, Je gharama hiyo inalingana na ile unayofikiria kuwatoza?)
Maswali haya yatakusaidia kujenga picha ya wateja unaotarajia kuwahudumia, huduma au bidhaa yako na bei zako pia. Hizi ni nguzo tatu muhimu sana katika biashara yako.
Ukiweza kupata majibu sahihi ya maswali hayo, basi utakuwa na wazo bora sana la biashara.
3. Umefanya Maandilizi gani utakapoanza kufanya biashara yako?
Kabla ya kuanza, kabla hata ya kufanya mauzo yako ya kwanza na kupokea mapato yako ya kwanza, swali la kwanza kujiuliza ni “utafanya nini na pesa zote utakazokusanya?”
Hapa ndipo shida na changamoto nyingi zitakapoanzia endapo utakuwa hujaweka misingi imara ya kuendesha biashara yako.
Mara kwa mara, nimekuwa naona na kusikia hadithi za kusikitisha kutoka kwa wafanyabiashara ambao hawakuweka misingi ya kuendesha biashara zao. Mfano; Taratibu na gharama za usafirishaji wa mizigo, huduma kwa wateja na uwekaji hesabu na mtiririko wa matumizi ya pesa au mapato yanayopatikana.
Mwisho wa siku, hujikuta wakipata hasara kubwa, pasipo kufahamu chanzo halisi cha hasara hizo.
Unaweza kudhani , labda haya mambo ni kwa ajili ya watu wenye biashara kubwa kubwa tu au kuhisi kama hakuna ulazima sana kwako.
Lakini unataraji kuwa mmiliki wa biashara, ni vyema ujue mapema kabisa kwamba hiki ni kitu unachopaswa kukiweka katika orodha yako ya mambo ya kufanya katika biashara yako. Weka kichwani kabisa!
HITIMISHO
Labda ungetamani kusikia ninakuambia, “Ukiweza kujibu maswali hayo matatu, basi kila kitu kitakuwa kimenyooka kwenye mstari na utafanikiwa haraka”, lakini kwa bahati mbaya katika ulimwengu wa biashara sivyo ilivyo.
Ukweli ni kwamba, utakuwa na siku nzuri na utakuwa na siku mbaya. Lakini, kwa sababu una kusudi linalokupa hamasa ya kusonga mbele, unatambua ni tatizo gani unaenda kulitatua na jinsi utakavyoshughulikia kila kitu baada ya kuanza biashara yako, basi utakuwa umeshinda nusu ya vita unayohitaji kupigana ili kuhakikisha biashara yako inafikia mafanikio makubwa.